Chicago
London
Dar Es Salaam
 
 

Mabinti Watanzania Wanavyotumikishwa Kwenye Madanguro China Part 2

News by : Staff Reporter
 
20 Jul, 2014 22:31:26
 
//
 
Munira baada ya kuamrishwa na ‘bosi’ wake kufanya kazi hiyo, alielekezwa na wenzake kwenda eneo la soko liitwalo Chambu Chambu ambako wanawake Watanzania wanafahamika kuwa maarufu kwa biashara ya ukahaba.
 

Binti huyo mwenye umri wa miaka 23 anasema usiku wa kwanza alipokwenda sokoni Chambu Chambu, wenzake walimkimbia, hivyo alichanganyikiwa na kuanza kuwapigia simu wenyeji wake kwani hakujua la kufanya.

 

“Nilimpigia simu Jacky na yeye alinijibu, ‘acha ujinga, tafuta hela uniletee mimi.” Anasema katika mazingira hayo alianza kulia na wakati akilia, alikutana na mwanaume wa Kinigeria, ambaye alimhoji maswali kadhaa.

 

Mnigeria yule alisema anaifahamu hoteli anayoishi Munira, lakini alimtaka wazungumze kwanza biashara kisha ampeleke na Munira alikubali.

“Nilizungumza naye biashara na tukakubaliana twende kwenye hoteli niliyofikia, baada ya kufanya mapenzi akanilipa  Dola 100, baadaye nilidakwa na mwenyeji wangu akinitaka nimpe fedha zote nilizopata,” anasema.

Alipomkabidhi fedha hizo, aliamrishwa kurudi tena sokoni kutafuta kiasi kingine cha fedha hadi atimize dola 200. Wakati huo bado ulikuwa ni mchana.

 

“Baada ya kumalizana na Mnigeria yule, nilienda kulala, lakini sikulala sana kabla mwenyeji wangu hajaniamsha na kuniambia lazima nitimize Dola 100 iliyobaki, hivyo nikanyanyuka na kwenda tena sokoni,” anasema.

Munira akawa hali wala halali vizuri akifanya kazi ya kujiuza mwili wake, kazi ambayo hata kiasi kidogo alichopata alitakiwa kugawana na mwenyeji wake kwa kumpatia Dola 200 kwa siku.

“Nilikuwa nachoka, hasa kwa kudaiwa, wakati mwingine nikiwa kwenye siku zangu najiuliza nitafanyaje ili nipate fedha za kulipa deni? Niliondoka hapa nikiwa na afya, lakini nilipofika huko baada ya muda mfupi niliisha, yaani niliisha,” anasema.

 

Ukatili wa aina yake

Anasimulia kwamba, siku moja  saa 10.00 usiku akiwa klabu,  alijisikia vibaya akatoka nje, akiwa huko alikutana na mwanamume ambaye walikubaliana wakastarehe kwa ujira fulani. 

Munira alikubali, lakini alijua kabisa kuwa anakwenda sehemu ambayo haifahamu kabisa. Baadaye aligundua kuwa eneo hilo linaitwa Nan-hai na linaongoza kwa matukio mengi ya uhalifu.

Anasema walikubaliana na mwanamume huyo wa Kinigeria na alikaribishwa na kuingia ndani katika nyumba yenye vyumba vinne, alipomuuliza iwapo anaishi peke yake, mwanamume huyo alimhakikishia kuwa anaishi peke yake.

 “Nikamwambia nataka kiasi fulani,  tukakubaliana niende Nan-hai, sehemu yenye matukio ya ajabu. Ni nyumba nzuri kwa kweli, nikaingia ndani, nikaoga,” anasema.

 

Baadaye Munira aligundua kuwa yule mwanamume anaishi na wenzake, wakati wanafanya tendo la ngono, alishangaa mwanamume mwingine anaingia chumbani na wote mmoja baada ya mwingine walimwingilia.

“Kwa kuwa nilikuwa nakataa kufanya walichotaka, walinipiga sana na ikabidi nikubali, hawakuniachia waliendelea kunibaka hadi kesho yake Saa 1.00 jioni, niliumia sana,” anasema.

Walimnyang’anya fedha alizokuwa nazo na  walipomuachia, mmoja kati ya wanaume wale alimpa Munira Yuan 100  na kumwambia hiyo ni nauli yake.

“Sikuelewa alikuwa na huruma au dharau?” anasema Munira. 

Munira anasema kuwa alichukua gari na kumpigia simu rafiki yake, ambaye alimpokea na walipoingia ndani alimsimulia kisanga kilichomkuta na kwa pamoja wakaanza kulia.

 “Rafiki yangu alinipeleka hospitali ambako nilipigwa ultra- sound na x-ray, ikaonyesha jinsi nilivyoharibiwa kwa kiasi kikubwa."

"Nikachomwa sindano za mishipa na kutundikiwa dripu, nilichomwa pia sindano za kuzuia maambukizi ya Virusi vya Ukimwi,” anasema.

Akiwa hospitalini hapo, Munira alikutana na  mwanamume mmoja Mnigeria ambaye  walizoeana kwa muda aliokuwa hapo Guangzhou.

Mwanamume huyo alipenda kumwambia Munira kuwa anafanana na mke wake.

Hata hivyo, Munira hawakumwambia Mnigeria huyo nini anachoumwa na badala yake walimdanganya kuwa anaumwa malaria.

“Alikubali akanisaidia kulipa bili ya hospitali, akaninunulia chakula na kunipa fedha nyingine ya ziada,” anasema.

 

Kutokana na mateso hayo,  aliamua kumpigia simu Josephine wa Magomeni (aliyemfanyia mipango ya kwenda huko)  kumwuliza kuhusu kazi yake, lakini Josephine alimtia moyo kuwa eti hoteli nyingi zimefungwa hadi msimu ujao.

“Kumbe kile nilichoambiwa na wenzangu kwamba kazi ni ukahaba, kikawa ndiyo hicho, niliamua kumwachia Mungu,” anasema.

 

Atuma picha

Akiwa hospitali, Munira alijipiga picha akiwa na majeraha aliyokuwa nayo na kuituma WhatsApp kwa baadhi ya watu ambao katika kutumiana ujumbe huo, hatimaye taarifa zilimfikia mwenyeji wake, Jacky.

“Aliponipigia simu hakuchukua hatua nyingine zaidi ya kuniuliza nipo wapi.  Nikamwambia nipo hospitali, basi akakata simu na wala hakutaka kujua zaidi kilichonisibu,” anasema.

Aliporudi hotelini,  Jacky alimwambia hataki kusikia suala lolote na wala hajali kama alikuwa anaumwa zaidi ya kutaka Dola 200 kila siku iendayo kwa Mungu.

 

Mwanadada  huyo anasema kutokana na mateso hayo, alikonda kiasi kwamba, ulipofika wakati wa kuongeza muda wake wa viza, (alikuwa ana viza ya mwezi mmoja), sura yake ilibadilika na ilitofautiana na picha iliyokwekwa kwenye viza.

Kwa bahati nzuri aliongezewa muda wa kuishi China kwa  siku 14 zaidi ili ajitayarishe kutafuta  kibali cha kuishi.

“Nilishangaa kusikia kwamba natakiwa niweke hela ya viza, kiasi cha Dola 300 na kiasi kingine Dola 200 za kumlipa mwenyeji wangu, wakati aliahidiwa kuwa atalipiwa kila kitu ikiwamo visa na malazi,” anasema.

Wakati huohuo, alitakiwa kulipia hoteli, ajinunulie chakula, atafute fedha ya viza, zile Dola 200 za kumpa mwenyeji wake  nazo zikabaki pale pale.

 

Viza inakwisha

Wakati hayo yanaendelea muda ulikuwa unapita na wiki mbili za nyongeza ya viza yake zilikuwa zinayoyoma.

Anasema ilikuwa ni bahati nzuri kwake kwani mteja wake mwingine pia mwenye asili ya Nigeria alimsaidia na kumpa fedha za  kuongeza muda  wa kuishi hapo Guangzhou.

Hata hivyo, alipokwenda kuongeza muda wa viza yake, alikutana na changamoto mpya pale maofisa uhamiaji, walipomwambia kwamba hawezi kupata kwani sura yake halisi ilikuwa inatofautiana kwa kiasi kikubwa na picha iliyopo kwenye viza, hivyo walimnyima kibali.

Wakati huo, muda wa viza yake ilikwisha kabisa na sasa alikuwa akiishi katika nchi hiyo kinyume cha sheria.

 

Itaendelea.....

 

SOURCE: Mwananchi

 
 
 
 
 
Copyright © 2011 Bongo Radio. Subsidiary of Bongo Media Group. All Rights Reserved
Valid XHTML 1.0 Transitional