Chicago
London
Dar Es Salaam
 
 

Idara Ya Uhamiaji Tanzania Yamwaga Ajira Kindugu

News by : Staff Reporter
 
28 Jul, 2014 23:42:15
 
//
 

IDARA ya Uhamiaji imekumbwa na kashfa nyingine ya kuajiri watoto na ndugu wa vigogo wa idara hiyo. Hayo yalibainika baada ya idara hiyo kutoa matangazo katika vyombo mbalimbali vya habari yaliyoonyesha majina ya waliofaulu usaili wa kutakiwa kujaza nafasi za konstebo na koplo wa Uhamiaji.

 

Tangazo hilo linaonyesha kuwa waliochaguliwa watatakiwa kuripoti makao makuu ya Uhamiaji Agosti 6.

 

Chanzo cha ndani cha habari ambacho hakikutaka jina lake litajwe, kilieleza kuwa kati ya watu waliochaguliwa, idadi kubwa ni watoto na ndugu wa maofisa wa Uhamiaji.

 

Kilieleza kuwa urasimu katika idara za serikali umeendelea ambapo hali inaonyesha kuwa bila kuwa na ndugu ni ngumu Mtanzania wa kawaida kupata ajira.

 

Chanzo hicho kilitaja majina ya walioitwa kazini na kubainisha uhusiano wao na watendaji waliopo idarani hapo ni Abdulhaq Amin Mandemla anayesadikiwa kuwa mtoto wa Ofisa Uhamiaji, Amin Mandemla na Alphonce E. Kishe anayedaiwa kuwa mtoto wa Ofisa Uhamiaji Aleluya Kishe.

 

Wengine ni Asha Burhan Idd, ndugu wa Ofisa Uhusiano Tatu Burhan Idd; Betrice Temba, ndugu wa Ofisa Uhamiaji Joseph Kasike na Geofrey Justine Mhagama, ndugu wa Ofsa Uhamiaji Rose Mhagama.

 

Aidha wamo Iginga Daniel Mgendi, mtoto wa Ofisa Uhamiaji Daniel Mgendi; Issack Michael Makwinya, mtoto wa aliyekuwa Ofisa Uhamiaji Makwinya; John Alfred Mungulu, mtoto wa Ofisa wa Uhamiaji Alfred Mungulu na Joseph A. Milambo ambaye ni mtoto wa karani wa Uhamiaji, Milambo.

 

Wengine ni Michael J. Choma, mtoto wa Ofisa Uhamiaji John Choma; Shimba H. Zakayo, mtoto wa Ofisa Uhamiaji Zakayo Mchele; Upendo Mgonja ambaye ni mtoto wa Ofisa Uhamiaji Mgonja na Vaileth A. Kidesu, mtoto wa Ofisa Uhamiaji Adam Kidesu.

 

Wamo pia Elizabeth Edward, ndugu wa Edward Martin; Ester Mahirane, ndugu wa Mahirane; Basil Lucian John, ndugu wa Ofisa Uhamiaji Dismas Lucian; Frank G. Kajura, ndugu wa Ofisa Uhamiaji Kajura na Jacob P Ulungi ambaye ni ndugu wa Ofisa Uhamiaji Magnus Ulungi.

 

Wengine ni Janeth John Millinga, ndugu wa aliyekuwa Ofisa Uhamiaji Millinga; Janeth R. Lukuwi, ndugu wa Ofisa Uhamiaji Eliza Lukuwi; Joseph N. Yondani, mtoto wa Ofisa Uhamiaji Mary Yondani; Leila Khatib Irovya, mtoto wa Msemaji Mkuu wa Idara ya Uhamiaji, Naibu Kamishna, Abbas Irovya.

 

Lucian F Mlula, ndugu wa Ofisa Uhamiaji Dismas Mlula; Neema Kasiano Lukos, ndugu wa Ofisa Uhamiaji Zubeda Abbas; Pendo Daudi Gambadu, ndugu wa Ofisa Uhamiaji Gambadu; Paschalia E. Mwenda, ndugu wa Ofisa Uhamiaji Martin Edward Mwenda.

 

Wengine ni Theresia Ernest Kalunde, mtoto wa Ofisa Uhamiaji Ernest Kalunde; Victor G. Mlay, mtoto wa aliyekuwa Ofisa Uhamiaji, Vitalis Mlay; Catherine J. Mapunda, mtoto wa Ofisa Uhamiaji Lucy Mapunda.

 

Gazeti hili lilimtafuta Ofisa Uhusiano wa Uhamiaji, Tatu Burhan, kufahamu ukweli kuhusu jambo hilo, lakini simu yake iliita bila mafanikio na hata alipotumiwa ujumbe mfupi wa maneno (sms) hakujibu.

 

Tanzania Daima Jumapili, liliwasiliana na Msemaji Mkuu wa Uhamiaji, Abbas Irovyi ambaye naye hakupatikana na simu yake haikuwa na majibu.

 

Naibu Msemaji wa Uhamiaji, Mbaraka Batenga, naye hakupatikana kama ilivyo kwa wenzake.

Tanzania Daima Jumapili, liliwasiliana na mmoja wa watedaji wa ofisi ya uhusiano, Juma Dau, ambaye alisema maofisa wengi wako nje ya nchi kikazi.

 

Hata hivyo, Dau, alisema yeye hana mamlaka ya kulizungumzia jambo hilo huku akilielekeza Tanzania Daima Jumapili, liwasiliane na Kaimu Msemaji wa Idara ya Uhamiaji, Batenga.

Itakumbukwa kuwa hivi karibuni Idara ya Uhamiaji ilitangaza nafasi za kazi 70 kwa wahitimu wenye shahada moja na kuendelea.

 

Ambapo awali majina ya maombi yalikuwa zaidi ya 20,000 na uongozi wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, ulipitisha majina ya waombaji 10,800 ili washindanie nafasi 70 tu katika usaili uliofanyika Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam Juni 13, mwaka huu.

 

SOURCE: Tanzania Daima

 
 
 
 
 
Copyright © 2011 Bongo Radio. Subsidiary of Bongo Media Group. All Rights Reserved
Valid XHTML 1.0 Transitional