Chicago
London
Dar Es Salaam
 
 

Vurugu Kubwa Zatokea Kwenye Tamasha La Diamond Platnumz Ujerumani

News by : Staff Reporter
 
03 Sep, 2014 03:25:05
 
//
 

Dar es Salaam. Mwanamuziki Diamond Platinum juzi alizua kizaazaa baada ya vurugu kubwa kutokea nchini Ujerumani na kuvuruga tamasha ambalo alitakiwa kutumbuiza, lakini meneja wake amesema tukio hilo litasaidia kumtangaza zaidi.

 

Vyombo vya habari vya Ujerumani vilitangaza vibaya vurugu zilizotokea baada ya Diamond, ambaye jina lake halisi ni Nassib Abdul, kuchelewa kufika ukumbini ambako baada ya kuwasili alishindwa kutumbuiza.

 

Meneja wake, Hamis Taletale alisema vurugu hizo zitamsaidia Diamond kujitangaza zaidi.

Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, meneja huyo alisema ingawa Diamond ameandikwa na kutangazwa vibaya katika vyombo vya habari nchini humo, hiyo kwake ni namna nyingine ya kujitangaza katika ulimwengu wa sanaa.

 

“Hivi sasa watu wengi nchini Ujerumani watakuwa wanamjua Diamond kwani baada ya kumsoma juu ya vurugu zilizotokea, watatafuta taarifa zake zaidi katika mitandao na pia kusikiliza na kutazama kazi zake,” alisema Taletale.

 

Taletale alisema kuwa kwa taarifa alizonazo mwenye makosa ni muandaaji wa tamasha hilo ambaye alichelewa kumfuata Diamond hotelini, hali ambayo iliamsha hasira za watu waliojitokeza katika tamasha hilo.

 

“Nasikitika sana kwa hili lililotokea. Siwezi kuwalaumu wale waliojitokeza na kufanya fujo. Hawa walikuwa na nia njema kabisa ya kumuunga mkono mwanamuziki wetu, lakini mwandaaji kwa sababu zake binafsi alichelewa kumfuata hotelini,” alisema Taletale.

 

Diamond alitakiwa kutumbuiza katika matamasha mawili nchini Ujerumani mwishoni mwa wiki iliyopita. Tamasha la kwanza lilipangwa kufanyika katika Mji wa Essen ambalo lilifanyika na siku iliyofuata alitakiwa kutumbuiza katika Mji wa Stuttgart, lakini vurugu zilikwamisha.

 

Diamond alishindwa kutumbuiza Stuttgart kwa sababu promota wa tamasha hilo raia wa Nigeria anayeitwa Britts alichelewa kumfuata kwani alikuwa umbali wa saa moja kutoka mahali ulipo ukumbi ambao ungetumika kwa tamasha hilo.

 

Taletale alisema ingawa mkataba ulionyesha kuwa mwanamuziki huyo alipaswa kupanda jukwaani saa 6:00 usiku, hakuweza kutoka kwa kuwa alikuwa ugenini.

 

“Unajua Diamond kule ni mgeni hivyo asingeweza kutoka hotelini mpaka afuatwe, cha ajabu mwenyeji wake ambaye ndiye aliyeandaa tamasha alimfuata saa 9:00 usiku, mpaka kufika ukumbini, tayari ilikuwa imeshafika saa 10:00 alfajiri.

 

“Diamond alipofika alikuta tayari wale watu wameanza kufanya fujo na polisi wamefika eneo la tukio. Inashangaza hata yule jamaa (Britts) alimwacha Diamond mpaka alipokuja kuondolewa na polisi mahali hapo,” alisema Taletale.

 

Watu waliojitokeza kushuhudia tamasha hilo walikuwa wamelipa kiingilio cha Euro 25 (Sh54,000) na walikuwa wametaarifiwa tamasha lingeanza saa 4:00 usiku.

 

Kwa upande wake, Diamond aliandika katika mtandao wa instagram akielezea kusikitishwa kwake na tukio hilo na kwamba halikuwa kosa lake.

“Napenda mashabiki wajue kuwa lile halikuwa kosa langu.”

 

SOURCE: Mwananchi

 
 
 
 
 
Copyright © 2011 Bongo Radio. Subsidiary of Bongo Media Group. All Rights Reserved
Valid XHTML 1.0 Transitional